Pages

Sunday, December 15, 2013

HIVI NDIVYO MANDELA ALIVYOPUMZISHWA KWENYE NYUMA YAKE YA MILELE HUKO QUNU

Mwili wa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela umelazwa katika nyumba ya milele leo (December 15), nyumbani kwao alikokulia katika kijiji cha Qunu, mkoa wa Eastern Cape, Afrika Kusini baada ya viongozi mbalimbali wa dini na serikali kutoa heshima zao za mwisho.
Mjane wake, Graca Machel, na Rais Jacob Zuma walihudhuria mazishi hayo ya kifamilia yaliyokuwa na mchanganyiko wa taratibu za kimila na za kisasa.
Jeneza lililobeba mwili wa Mandela lilibebwa na wanajeshi, na kusindikizwa na wana familia na marafiki hadi katika eneo la kaburi.
Ndege za kivita za Afrika Kusini zilitoa heshima za mwisho kwa kuzunguka juu ya anga huku mizinga 21 ikipigwa wakati mwili wa Madiba ukishushwa kwenye nyumba yake ya milele.
Wakati jeneza la hayati Mandela likiteremshwa kaburini, bendera ya Afrika Kusini iliyokuwa imelifunika iliondolewa na kukabidhiwa kwa mjane wa Mandela mama Graca Machel.
Hata hivyo vyombo vya habari havikuonesha jinsi mwili huo ulivyokuwa ukiingia kaburini kwa kuwa familia yake iliomba sehemu hiyo ya mazishi isioneshwe.
Mazishi hayo yamehudhuriwa na wageni wapatao 5,000 waliopewa mwaliko wakiwemo familia, viongozi mbalimbali na watu maarufu. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete pia amehudhuria mazishi hayo.
Wengine walioalikwa ni pamoja na malkia wa talk show Oprah Winfrey aliyeongozana na mpenzi wake Stedman Graham, mke wa zamani wa Mandela Winnie Madikizela, Askofu Desmond Tutu, Prince Charles wa Uingereza, Rais wa Malawi Joyce Banda na wengine.
Wanakijiji wa Qunu ambao hawakupata mwaliko walishuhudia safari ya mwisho ya shujaa wao kupitia TV kubwa iliyowekwa pembeni kidogo kutoka sehemu ambapo shughuli ya mazishi ilipokuwa ikifanyika.
Nelson Mandela alizaliwa July 18, 1918 na kufariki  December 5, 2013 akiwa na umri wa miaka 95.
Apumzike kwa amani Nelson Rolihlahla Mandela.

0 maoni:

Post a Comment

Matangazo

Matangazo

Popular Posts

 

Blogger news

Blogroll

About