Pages

Thursday, October 17, 2013

HII NDIO KAULI YA ZITTO ILIYOVIKOROGA VYAMA VYA SIASA....VYAMA VYAHAHA KUELEZA USAFI WAO


*Vyama vyahaha kuelezea usafi wa hesabu zao kabla ya kunyimwa ruzuku

KAULI ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaka kusitishwa utoaji ruzuku kwa vyama vya siasa hadi pale hesabu zao zitakapokaguliwa, inaonekana kuwachanganya viongozi wa vyama hivyo.

Zitto alisema jijini Dar es Salaam juzi kwamba jumla ya Shilingi bilioni 67.7 zimetolewa na Serikali na kupewa vyama tisa vya siasa, lakini hadi sasa hesabu zao hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka na kusema hesabu zao ziko makini, kwani zimekaguliwa na wakaguzi wa hesabu wa nje kwa maelekezo ya CAG.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM imekuwa ikitekeleza utaratibu wa kukaguliwa hesabu zake tangu mwaka wa fedha 1977/78 kilipoanzishwa hadi 2003/4, ambapo hesabu zao zilikuwa zikikaguliwa na Tanzania Audit Corporation (TAC).

Alisema hesabu za chama hicho kikongwe cha siasa barani Afrika ziliendelea kukaguliwa na Januari 29 mwaka huu, CCM ilimwomba CAG awapangie mkaguzi wa hesabu za 2011/2012, CAG akawapangie kampuni ya TAC-Associates, kampuni itakayoendelea kukagua hesabu za CCM hadi 2013/2014.

“Hesabu zilizokaguliwa zote zipo kwa CAG na za 2011/2012 ziko mikononi mwa TAC-Associates, wakimaliza zitawasilishwa kwenye vikao vya chama na baadaye kwa CAG,” alisema Nape. 

Nape aliitetea CCM dhidi ya kauli ya Zitto ya kuzuia kupewa ruzuku na kwamba wapo tayari kukutana na PAC.

“Huenda kauli ya Zitto imekilenga chama chake mwenyewe kinachodaiwa kufanya matumizi mabaya ya fedha za ruzuku kwa viongozi wake kukopeshana bila kufuata utaratibu,” alisema.

Zitto ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza na RAI kuhusu kukaguliwa kwa hesabu za CCM, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alionyesha kushangazwa na kauli za Nape kuhusu hesabu za chama hicho tawala.

Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Chadema alisema kuwa CAG hana hesabu za CCM, na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote kitakachopata ruzuku hadi baada ya kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu za kipindi cha miaka minne.

“Kama CCM wanasema wamefanyiwa ukaguzi, basi hesabu zao zimekaguliwa na mkaguzi wa kichochoroni. CAG hazijui, hana taarifa za hesabu za CCM kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Hayo ni makosa, na si wao tu, bali vyama vyote vinavyochukua fedha za walipa kodi wa Tanzania na kuzitumia hovyo, havitapata tena ruzuku hizo,” alisema.

Awali, Zitto alitoa agizo hilo baada ya kamati yake kumaliza mkutano wake na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi jijini Dar es Salaam, akisema hesabu hizo ni za kuanzia mwaka wa fedha wa 2009/10.

Vyama hivyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP, APPT Maendeleo na Chausta.

Jana Nape alimshambulia moja kwa moja Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, akitaka awajibike kutokana na kile alichodai kuwa ni ufujaji mkubwa wa fedha ndani ya Chadema, chama kikuu cha upinzani.

“Sote tunafahamu kuhusu kelele zilizopo mtaani juu ya matumizi mabaya ya ruzuku Chadema. Wanachama kule wanalalamika sana na kuwalaumu viongozi wao. Si ajabu hawa jamaa wakawa wanakiuka sheria hii. Zitto awashughulikie wao kwanza,” alisema Nape.

Zitto hakushitushwa na kauli hiyo ya Nape na aliliambia RAI kwamba, anachokifanya ni kutimiza wajibu wake kama Mwenyekeiti wa PAC na wala si kumkonoa yeyote ndani au nje ya Chadema.

“Vyama vyote vitakaguliwa ikiwa ni pamoja na Chadema. Ukweli utajulikana na kama kuna hatua zitachukuliwa. Si kukomoana,” alisisitiza Zitto.

Hata hivyo, RAI lilidokezwa na mwanachama mmoja wa Chadema kwamba kumekuwapo na mitafaruku ya chini kwa chini ndani ya Chadema kuhusu matumizi ya fedha, iwe za ruzuku au misaada kutoka kwa wafadhili.

Chanzo cha uhakika kutoka Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Mfipa, Kinondoni ambacho ni wazi hatuwezi kukianika hadharani, kilisema kuna fedha nyingi zilizotolewa kwa ajili ya mikutano ya Vuguvugu la Mabadililo (M4C) lakini hazikutumika kama ilivyokusudiwa.

Mtoa taarifa wetu alidai kuwa posho na marupurupu ya viongozi kadhaa na wake zao ni za kutisha na kutia shaka hesabu za chama hicho hata kabla PAC haijataka kukaguliwa kwake.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro akizungumzia suala hilo la ukaguzi wa hesabu alisema huenda Katibu wa Bunge haijapewa taarifa sahihi kuhusu chama hicho, akidai kuwa kiliandikiwa barua ya kutakiwa kufanyiwa ukaguzi kwa sharti la kumlipa CAG.

“Ilikuwa mwaka 2011 CAG alipotuarifu kuwa kuna taasisi imeteuliwa kwa ajili ya kufanya ukaguzi, tukauliza inakuwaje kazi inayofanyika ni ya Serikali sisi tumlipe mkaguzi?

“Hofu yetu ilikuwa kwamba tungeweza kutuhumiwa kumuhonga mkaguzi huyo. Sasa huenda Zitto hajapewa taarifa sahihi kabisa,” alisema Mtatiro. 

Kwa mujibu wa sheria, CAG analo fungu lake kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kamwe hapaswi kulipwa na mteja anayekaguliwa.


Wadadisi wa mambo wanasubiri kwa hamu kuona ninikitatokea ndani ya vyama hivyo vikubwa vya siasa nchini; CCM, Chadema na CUF kama vikishindwa kuhalalisha matumizi ya fedha za ruzuku walizopewa.

0 maoni:

Post a Comment

Matangazo

Matangazo

Popular Posts

 

Blogger news

Blogroll

About